Sunday 27 April 2014

MUUNGANO: Zanzibar Jaji mmoja Mahakama ya Rufaa




Jaji Mkuu  Zanzibar Othman Omar Makungu akizungumzia changamoto na matatizo mbalimbali yanayoikabili idara ya Mahakama Zanzibar, ikiwamo  uchache wa Wazanzibar kwenye Mahakama ya Rufani Tanzania. Picha na Mwinyi Sadallah 

  Mahakama ya Rufaa imekuwa mkombozi wa kesi nyingi za Zanazibar na kutenda haki kwa raia wengi.
Zanzibar. Wakati Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ukiadhimisha miaka 50,  Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu anasema bado kuna tatizo la uhaba wa majaji kutoka Zanzibar katika Mahakama  ya Rufani Tanzania.
Jaji Makungu anasema hivi sasa Mzanzibari amebaki mmoja katika mahakama ya Rufani ambaye ni Jaji Mbarouk Saleh, baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhan kustaafu, jambo ambalo anasema linahitaji kuwekewa mipango maalumu ili kuwajengea uzoefu wanasheria waliopo waweze kuingia kwenye mahakama hiyo.
Hata hivyo anasema tatizo hilo lilitokana na siku za nyuma Zanzibar kukabiliwa na uhaba wa wanasheria na wakati mwingine kulazimika kuajiri kutoka Nigeria au Tanzania Bara, ambapo sasa hali hiyo iko tofauti, ila tatizo linalobaki ni kukosekana uzoefu wa kuingia kwenye mahakama za juu.
Jaji Mkuu huyo anasema Mahakama ya Rufani Tanzania inahitaji kuwa na majaji wenye uzoefu wa kutosha katika mambo ya sheria, kutokana na uzito wake wa kuwa chombo cha mwisho cha maamuzi kwa mujibu wa katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Anasema sheria inaruhusu kuteuliwa wanasheria kutoka nje ya mfumo wa mahakama kama hakuna watu wenye uzoefu katika Idara ya Mahakama, na kuongeza kusema kuwa ni vizuri majaji wakawa wamepitia katika mfumo wa mahakama kabla ya uteuzi wao.
“Tuna tatizo la uhaba wa majaji katika Mahakama ya Rufani, wengi tuliokuwa nao uzoefu wao bado ni mdogo katika mahakama hiyo,” anaeleza Jaji Makungu.
Anaeleza katika miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mahakama ya Rufani imekuwa ni chombo chenye mafanikio kinachosimamia haki za raia, kwa kuwa tangu kuanzishwa kwake imeongozwa na majaji wenye ujuzi na uzoefu.
 Jaji Makungu anasema ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar umekuwa ukiimarika katika nyanja za mafunzo, kubadilishana uzoefu. Mahakama Kuu na mahakama za chini hazimo kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
Anasema mahakama ya Rufani imekuwa ikikutana Zanzibar mara moja kwa mwaka, kati ya Novemba na Desemba ratiba ambayo alisema haihitaji kuangaliwa upya, licha ya kuwepo malalamiko ya wananchi kuwa utaratibu huo huchelewesha upatikanaji wa haki kwa muda mwafaka.
“Kama mtu ana shauri lake, anaweza kukata rufaa kwa kutumia haki ya dharura na ombi lake likasikilizwa Dar es Salaam, kama anahisi hakuna uharaka ana uwezo wa kukata rufaa kwa utaratibu wa kawaida na kusubiri Mahakama ya Rufani inapokutana Zanzibar na shauri lake kuamuliwa,” anafafanua Jaji Makungu.
Anabainisha kuwa Zanzibar itakabiliwa na changamaoto endapo rasimu ya pili ya Katiba itapitishwa na Bunge Maalumu la Katiba na kuidhinishwa kwa mahakama ya juu mbali ya Mahakama ya Rufani Tanzania, kwa vile Zanzibar itahitaji kutoa majaji wasiozidi watatu ili kuingia katika mahakama hiyo.
Anaeleza kuwa hivi sasa Zanzibar ina wanasheria wa kutosha ingawa bado hawajawa na uzoefu na kuwataka wanasheria kuzingatia majukumu  mbalimbali katika utekelzaji wa kazi zao, ili sifa na vigezo vya uzoefu viweze kufanana na kazi wanazozifanya
Mwananchi..


Unknown Web Developer

No comments:

Post a Comment