Sunday, 27 April 2014

Tukio la kuchanganya udongo wa Muungano na miujiza yake




Mwalimu Julius Nyerere  akichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar kuashiria Muungano wa nchi hizo mbili, na yeye kuwa Rais wa Kwanza wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania
Uteuzi na kupende-kezwa majina ya vijana 100 kutoka Zanzibar ambao waliungana na wenzao wa Tanganyika ulifanywa na Halmashauri Kuu ya ASP Youth League,  wiki moja kabla ya siku ya Muungano walichezeshwa gwaride la Muungano, nyakati  za asubuhi na jioni wakiongozwa na Bi Mwakemwa.
Kazi ya kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar ilianza saa tatu asubuhi na kulikuwa na miujiza mingi.
Zanzibar. Wakati  Watanzania wakiadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,  siku ulipochanganywa udongo wa pande mbili za Muungano kulikuwa na mazingira ya ajabu na mabadiliko ya vipindi vya hali ya hewa vilivyowababaisha na kuwashangaza watu wengi waliohudhuria sherehe hizo.
Sherehe za kuchanganya udongo wa pande mbili uliowekwa kwenye vibuyu viwili tofauti zilifanyika Aprili 26, 1964 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Mwalimu Nyerere alichanganya udongo kwa kuumimina ndani ya chungu kuashiria Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mmoja kati ya watu  waliobeba udongo wa Zanzibar na kuchanganywa na ule wa Tanganyika,  Hassan Omar Mzee (66) akihojiwa na Mwananchi nyumbani kwake huko Kibweni nje ya Mji wa Unguja, anaitaja siku hiyo ilikuwa ya aina yake atakayoikumbuka maishani. Wakati wa tukio hilo alikuwa na  umri wa miaka 16.
Hassan anasema kazi ya kuchanganya udogo wa Tanganyika na Zanzibar ilianza  saa tatu asubuhi na kukiwa na manyunyu ya mvua, jua lisilounguza likiwaka na kupotea na mawingu yaliyokuwa na kivuli  cha ubaridi yakiwa yametulizana juu ya anga huku ukimya ukitawala eneo la uwanja.
Anasimulia kuwa lilikuwa tukio la aina yake ambalo liliwashangaza viongozi wengi wa nje na ndani, waliohudhuria na kushuhudia kitendo hicho cha kijasiri na cha kihistoria kilichofanywa na viongozi wa mataifa ya Tanganyika na Zanzibar, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume (wote kwa sasa ni marehemu).
Mshangao huo unatokana na mazimio ya harakati za vikao vingi vya viongozi wa Kiafrika, walikuwa na lengo la kuungana baada ya kujikomboa kutoka kwenye ukoloni, lakini  maazimio hayo yaliwashinda viongozi wengi  pia Nyerere na Karume walitekeleza kwa vitendo.
Anasema siyo Mwalimu Nyerere wala Mzee Karume walionekana kuwa na hofu ya kupoteza madaraka ya nchi zao, hawakutaka kuendekeza fahari ya vyeo vyao na badala yake walichokitanguliza mbele ni  nia na azma ya kujenga umoja wa kitaifa wa watu wao.
Jamhuri ya watu wa Zanzibar na ile ya Tanganyika ndipo zilipokufa. Mabeberu na wakoloni wakipigwa na butwaa kuona kitendo hicho kikitokea na viongozi wa pande mbili wakiwa na nyuso za furaha na bashasha pia wananchi wengine wakionekana kutokwa na machozi ya furaha kutokana na tukio hilo.
Akielezea tukio hilo, Hassan anawataja wenzake wengine watatu walioshiriki katika kazi ya kubeba udongo wa pande mbili za Muungano  ni Hassan Kheir Mrema na Sifaheri Kunda kutoka Tanzania Bara na Khadija Abbas kutoka Zanzibar.
Wenzao wanawake walibeba vibuyu vidogo na vikubwa vyenye udongo na wanaume walibeba chungu kimoja kilichochanganyiwa udongo, tukio lilifanyika katikati ya Uwanja wa Taifa ambako jukwaa maalumu lilijengwa.
“Siku hiyo tuliamka mapema tukiwa tumepewa mavazi maalumu, wanaume tulivaa shati na suruali zilizoshonwa kwa vitenge, wenzetu wa kike walivaa mavazi maalumu ya khanga zilizozingatia utamaduni wa Mwafrika,” anaeleza Hassan.
Mwananchi.
Unknown Web Developer

No comments:

Post a Comment