Thursday 6 August 2015

TUNAHAMA KWA MPIGO




MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Elias Ngorisa, (Katikati, akizungumza kwa niaba ya madiwani 18 wa kutoka CCM, wilayani humo, wambao wamejivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na CHADEMA Agosti 5, 2015. Madiwani hao walipokelewa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mh. Joshua Nasari, (wapili kushoto).  

NA K-VIS MEDIA
WIMBI la wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, CCM, kukihama chama hicho linazidi kukua, ambapo Agosti  5, 2015,  madiwani 18 wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, akiwemo mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elias Ngorisa  wamejivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Akiwawakilisha madiwani hao waliohama, Ngorisa aliyeambatana na Katibu wa fedha na uchumi wa CCM wilayani humo, Kagil Ngukwo, ambaye alikuwa diwani wa Kata ya Engusero Sambu, walikabidhiwa kadi mpya wa CHADEMA na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari maarufu kama “Dogo Janga”.
Pia wazee wa kimila wa Kabila la Kimasai (malaigwanani) Lekakui Oleiti na Laurence Ngorisa, wote kutoka Engusero Sambu, walihudhuria tukio hilo la kujiunga na CHADEMA.
Akizungumza wakati wa tukio hilo la kupokea kadi za CHADEMA,  Ngorisa, alisema wapo madiwani 18 kati ya 28 ambao tayari wamechukua kadi za Chadema.
“Leo (jana) tumewawakilisha hapa, lakini wamekwishakihama Chama Cha Mapinduzi…madiwani hao watatetea nafasi zao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
“Nimeshawishika kwa dhati kabisa kubadili mwelekeo wa awali na kuwa mwanachama wa Chadema.
“Sisi tumehamia CHADEMA kwa vile tunataka mabadiliko na mjuelekeo ulivyo mabadiliko yako huku CHADEMA na sio CCM.” Alisema  Ngorisa.
“Kilichotusukuma kuhamia CHADEMA, ni kumuunga mkono mgombea wa kiti cha Rais wa Tanzania kupitia UKAWA Mh. Edward Lowassa.”
Tangu atangaze kukihama chama cha Mapinduzi mwishoni mwa mwezi uliopita, Mh. Edward Lowassa, alisema, uamuzi aliouchukua ni mgumu kwa vile nia yake ya kuwaondolea umasikini Watanzania bado iko palepale, na kwa vile anatambua Watanzania wanataka mabadiliko, basi mabadiliko hayo yatapatikana nje ya CCM.Tayari madiwani wengine kadhaa wa wilaya ya Monduli, wamekwisha ihama CCM muda mfupi baada ya mkutano mkuu wa CCM uliomalizika mwezi uliopita mkoani Dodoma, wakisema kuwa hawakuridhishwa na mchakato wa kumpata mgombea wa kiti cha Rais wa Tanzania kupitia chama hicho, ambapo, aliyekuwa Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani Mh. Edward Lowassa, alikatwa jina lake katika hatua za awali za vikao vya chama hicho
Unknown Web Developer

No comments:

Post a Comment