Sunday 9 February 2014

Wacomoro hoi kwa Yanga, walala 7-0



Kikosi cha timu ya Yanga ya Tanzania

Michuano ya kuwania kombe la klabu bingwa Afrika imeanza kutimua vumbi, ambapo mabingwa wa Tanzania, Dar es Salaam Young Africans,"Yanga", wameicharaza kikatili klabu bingwa ya Comoro, Komorozine, magoli 7-0.
Mchezo huo wa hatua ya awali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika, ulipigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Jumamosi, timu ya Yanga ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0 hadi dakika 45 za kwanza. Magoli hayo yalifungwa na mshambuliaji Mrisho Ngassa katika dakika ya 13 na dakika tano baadaye Nadir Haroub Cannavaro, akipachika goli la pili. Kipindi cha pili ndicho kilikuwa mvua ya magoli na kuonekana wageni kushindwa kumudu kasi ya wachezaji wa Yanga ambao walikuwa na uchu wa magoli.
Mrisho Ngassa aliweza kupachika mabao mawili zaidi huku Didier Kavumbagu akipachika magoli mawili na Hamis Kiiza akipachika moja na kufanya mchezo huo kukamilika dakika 90 kwa wenyeji Yanga kupata ushindi mnono wa mabao 7-0
Timu ya Yanga ikifanikiwa kushinda tena katika mchezo wa marudiano, huko Comoro wiki mbili zijazo, basi itakwaana na mabingwa wa Misri, Al Ahly katika mchezo wa raundi ya kwanza.
Katika mchezo mwingine timu ya Kampala City Council ya Uganda iliibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Al Merreikh ya Sudan. Huku Gor Mahia wakiilaza US Bitam ya Gabon 1-0
KWA HISANI YA BBC SWAHILI.
Unknown Web Developer

No comments:

Post a Comment