Sunday 27 April 2014

Kingunge apinga matusi, kejeli dhidi ya Warioba




Dodoma. Mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru amekemea kauli za kejeli na matusi dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba, alisema wanaombeza Warioba wanapaswa kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa hawamtendei haki.
“Siyo sawa hata siku moja kumshambulia Warioba eti kwa sababu ya misimamo yenu ya vyama, hata mimi japo nimestaafu lakini bado ni mwanaCCM kwa hiyo tabia hii ni mbaya na haileti heshima,” alisema Kingunge.
Alisema kuwa misimamo ya vyama inapotokea kuwatukanisha watu tena wenye heshima zao inakuwa ni aibu kwa chama pamoja na jamii kwa jumla na inaondoa heshima ya mtu.
Kauli ya Kingunge imekuja zikiwa zimepita siku chache baada ya kujitokeza kwa hali ya mashambulizi ya matusi ndani ya Bunge ambayo yalikuwa yakielekezwa kwa Warioba kuhusu tuhuma za kuchakachua maoni ya wananchi.
Tuhuma za hivi karibuni zilitoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia ambaye alimtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani kufunga mdomo wake kwa kuwa kazi yake imekwisha.
Mbali na huyo, Mbunge wa Mbinga Mashariki, John Komba alimfananisha Warioba na Adam na Hawa ambao waliasi katika Bustani ya Edeni.
Akizungumzia Rasimu, mkongwe huyo alisema Katiba haitapatikana pasipokuwapo na maridhiano na makubaliano na akawataka wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba warudi bungeni ili waweze kujadiliana na kutengeneza katiba ya wananchi.
Kingunge aliwasifia waganga wa tiba za jadi kwa kumpendekeza kama mlezi wao tangu 1998 ili aweze kuwawakilisha hivyo akasema hakubebwa wala kupita njia za panya kama ambavyo wengine wanasema.
Pinda awaomba Ukawa warudi bungeni
Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana alitumia dakika 13 alizopewa na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kuwaomba wajumbe wa kundi la Ukawa kurejea bungeni ili waweze kukubaliana katika utungwaji wa katiba ya wananchi.
Pinda alisema, “Yaliyopita si ndwele, naomba nitumie nafasi hii kuwasihi sana hawa ndugu zetu waliosusia Bunge, warudi tukubaliane pamoja katika kutengeneza katiba ya wananchi.”
Mwananchi.
Unknown Web Developer

No comments:

Post a Comment