Tuesday, 22 April 2014

MAREHEMU MOSHI CHANG'A ATAZIKWA KESHO IRINGA.




Dar/Rukwa. Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Moshi Chang’a aliyefariki dunia juzi atazikwa kesho Kihesa mkoani Iringa.
Chang’a alifariki juzi saa 10.15 jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa tangu Machi 29, mwaka huu kwa ugonjwa wa shinikizo la damu.
Mdogo wa marehemu, Faustine Kikove alisema jana kwamba mwili wa marehemu utasafirishwa leo saa 10.00 jioni kwa gari kwenda Iringa.
Alisema kabla ya kusafirishwa, mwili wa Chang’a utaagwa nyumbani kwake Mbagala Kibondemaji kuanzia saa 8.00 mchana na utazikwa kesho baada ya swala ya adhuhuri.
Akimzungumzia marehemu, alisema wakati akiwa Kalambo, alimpigia simu akimweleza kuwa hajisikii vizuri na kwamba alikuwa anakwenda Muhimbili kwa ajili ya kuchunguza afya yake.
“Hatukujua kwamba hali yake ingebadilika ghafla, tulijua anakwenda kuchunguzwa afya na angerejea salama kuendelea na majukumu ya kitaifa lakini haikuwa hivyo,” alisema .
Akizungumzia kifo hicho, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alisema ni pigo kwa Wanakalambo na mkoa mzima kwa jumla.
“Tumepoteza kiongozi ambaye alikuwa mwongoza njia ambaye wananchi aliowaongoza walimpenda kwa ucheshi wake na uchapakazi,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema katika vikao vya wakuu wa wilaya, Chang’a alikuwa mwalimu kutokana na uzoefu wake wa kutumikia nyadhifa mbalimbali za Serikali.
“Alitufundisha mambo mengi kutokana na uzoefu wake, pia kwa sababu ni mwalimu kitaaluma na kiongozi wa muda mrefu CCM,” alisema Rugimbana.
Nyumbani kwa marehemu viongozi walifika kutoa pole kwa wafiwa, wakiwamo Manyanya na Rugimbana ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwas
Mwananchi.
Unknown Web Developer

No comments:

Post a Comment