Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji Peter Msigwa amemvaa
Askofu Donald Mtetemela na kumtaka avae rasmi magwanda ya Chama cha Mapinduzi
(CCM).
Akizungumza na gazeti hili, Msigwa
ambaye pia ni Mbunge kupitia Chadema alisema Askofu Mtetemela alionyesha
upendeleo wa wazi kwa CCM alipokuwa akichangia bungeni mjini Dodoma Alhamisi
iliyopita.
Katika mchango wake, Askofu
Mtetemela alikemea tabia ya wajumbe wa Bunge hilo kuwakashifu waasisi wa Taifa
aliosema wana heshima kubwa kwa jamii na mbele za Mungu.
Hata hivyo, Msigwa alisema:“ Askofu
ameonyesha upendeleo wa wazi wazi japokuwa anasema anasimamia katikati (hana
upande kisiasa). Hakuona kejeli, ubaguzi na matusi yaliyokuwa yakiendelea ndani
ya Bunge?”
Mchungaji Msigwa alisema yeye ni
mchungaji lakini amejitokeza wazi kusimamia Chadema tofauti na askofu huyo
ambaye ameonyesha wazi upande anaousimamia wa CCM, wakati awali walidhani ni
mtu mwenye msimamo wa kati.
“Mimi sina ugomvi kama ameamua kuwa
mwanasiasa kama mimi lakini awe wazi kwa kusimama na kujionyesha wazi upande
aliopo,”alisema.
Kauli ya Askofu Mtetemela
Katika mchango wake, Askofu
Mtetemela alilieleza kukerwa na kauli ya Profesa Lipumba kuliita Bunge la
Maalum la Katiba kuwa linafanana na kundi ovu la Italahamwe.
“Nasikitika kwamba sijaweza kumuona
yeye binafsi Profesa Lipumba ili niweze kumwambia masikitiko yangu, na naamini
ni masikitiko ya wengine. Mshtuko wangu ni kwamba alilinganisha Bunge hili na
kundi la Intarahamwe la Rwanda,” alisema.
Alibainisha kwamba kihistoria
inajulikana Intarahamwe ni wauaji, hivyo sio busara kabisa kuwafananisha
wajumbe wa Bunge Maalumu na kundi hilo.
“Hatuko hapa kumuua mtu yeyote,
kutuita sisi wauaji si jambo jema, ni baya lakini pia kauli hiyo inaweza kufufua
maumivu ya wenzetu wa Rwanda ambao hawataki hali hiyo ijirudie tena katika nchi
yao,” alisema.
Alieleza kuwa kauli hiyo pia inaweza
kuibua hisia tofauti hata kwa Serikali ya Rwanda inayoweza kufikiri kuwa
Tanzania inalifanyia mzaha jambo lililowaumiza kwa kiasi kikubwa.
Aidha alisema: ‘’ Wajumbe wamekuwa wakikosa heshima mbele ya
viongozi wao na kuvunja kanuni kama wanavyotaka wenyewe, jambo ambalo ni hatari
zaidi kwani linaweza kusababisha mvurugano.’’
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment