Watanzania wengi wamejenga tabia ya kunywa dawa za Malaria bila kupima afya zao na huku wakikosa huduma sahihi hali ambayo inaelezwa kuchangia kuenea kwa vimelea vya ugonjwa huo na kusababisha usugu wa dawa.
Hilo linasababishwa na wengi kujijengea mazoea ya kununua dawa bila kupima au kuandikiwa dawa na madaktari ambao hawajahakikisha kwa vipimo kama kweli wana malaria.
Hali hii inatajwa kuwaweka wagonjwa katika hatari ya kupoteza maisha kutokana kutopata tiba sahihi kwa wakati.
Wapo watu ambao hawana utamaduni wa kwenda hospitali kwa ajili ya kujua afya zao bali pindi wanapojisikia homa, hukimbilia kunywa dawa za malaria bila kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu.
Hilo limethibitishwa na mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Profesa Nicodemus Govela ambaye amekiri kuwepo na utamaduni wa madaktari kusikiliza dalili za mgonjwa na kufikia uamuzi wa kutoa dawa bila kumpima.
Anasema wapo baadhi ya madaktari ambao licha ya kumpima mgonjwa na kugundua kuwa hana malaria, lakini hutoa dawa kwa kubashiri huenda ikawa imejificha kulingana na maelezo anayopewa.
“Wapo madaktari ambao hufanya uamuzi wao kwa kuotea, utakuta anampima mgonjwa na kukuta hana malaria, lakini kwa kusikiliza maelezo ya mgonjwa na kwa uzoefu wake anaamua kumpa dawa, kitu ambacho kinaweza kusababisha madhara makubwa,” anasema.
Wataalamu wa afya ambao wanapaswa kuwa kimbilio la wagonjwa, kwa namna fulani wamekuwa kichocheo cha kuenea kwa ugonjwa huu kutokana na uzembe ambao umekuwa ukifanywa na baadhi yao.
Watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa kuna wakati hawapati vipimo sahihi lakini wanaambiwa kuwa na vijidudu vya malaria na kuanzishiwa dawa za kutibu ugonjwa huo bila ya kuthibitishwa.
Profesa Govela anasema: “Mtu akiwa na homa basi daktari anakimbilia kumpa dawa ya malaria bila kuthibitisha kuwa homa hiyo inaweza kuwa sababu ya ugonjwa.”
Anaongeza kuwa hali hiyo pia inasababishwa na uvivu wa madaktari kwa kushindwa kufikiria sababu nyingine za homa kwa mgonjwa hivyo kupeleka mawazo yao moja kwa moja kwenye malaria.
Anasema vipo vyanzo mbalimbali vinavyosababisha mtu kupata homa, hivyo ni jukumu la daktari kujaribu kutafuta sababu za homa kwa mgonjwa na siyo kukurupuka kutoa dawa za malaria.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment