Thursday 9 April 2015

UCHAMBUZI WA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO, 2015




UCHAMBUZI WA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO, 2015

UTANGULIZI

Sheria hii ya Makosa ya Jinai kupitia Mtandao, 2015 ina mapungufu mengi. Mapungufu hayo yamebainika kuwa, kama sheria ikipita yanaweza kuifanya nchi ikawa ni kati nchi adui za matumizi ya mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano duniani.

Watanzania wote wanatakiwa kufahamu kuwa muswada ukipita utatumika nchini kote yani Tanzania Bara na Visiwani.

Watanzania walio wengi hawafahamu Sheria hii inawahusu kwa namna gani; lakini kwa lugha rahisi ni kuwa itamuathiri mtu yeyote anayeweza tumia Mtandao wa Intaneti kwa kutimia kifaa chochote iwe kompyuta kubwa au vifaa vyenye uwezo wa kufanya kazi kama kompyuta kama Simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyoendana na hivyo.

Malengo ya Sheria hii ni kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.

Matumizi ya mitandao yote mikubwa kama Twitter, Instagram, JamiiForums, Facebook, Barua pepe, WhatsApp, blogu na data zote zilizo katika kifaa chochote cha kielektroniki yanaathiriwa kwa kiwango kikubwa na Muswada huu.
UCHAMBUZI

Kifungu cha 7
(1-3): Haibainisha ni aina gani za data ambazo haziruhusiwi kuguswa/kufutwa au zikiguswa/futwa ni kosa la jinai.

7(1g): Kipengele hiki katika kifungu hiki kinarudiwa mara kadhaa katika (Vifungu vya 32-35). Badala ya vifungu vya mbele kurejea kifungu hiki, watunga sheria wameiacha kifungu hiki kikiwa hakieleweki hadi mtu asome vifungu vya mbele.

Je mtu aliyeidhinishwa katika ibara na kipengele hiki ni nani?

Kifungu cha 8:
Muswada huu haujaweka bayana iwapo nyaraka za siri zinaweza kuwekwa wazi katika mtandao kama zina maslahi ya nchi au wananchi mf. Matumizi mabovu ya pesa za umma

Kifungu cha 14:
Neno pornografia halijapewa maana na hivyo jambo lolote lenye mwonekano wa kiasherati (sexually vulgar) linaweza kutafsiriwa kama pornografia na kumuingiza muhusika matatizoni.

Ponografia ya mtandao isikatazwe kabisa ila inatakiwa kuweka ulinzi thabiti wa kuhakikisha watoto hawawezi kufungua mitandao ya aina hiyo.

Ponografia zote ni chafu lakini sio chafu zote ni ponorafia. Hivyo kutokana na kuwa sheria hii inasema ponografia zote ni chafu hii itasababisha kila mtu ahukumiwe chini ya kifungu B.

Uchafu na Ponografia viwe vipengele viwili tofauti.

Kifungu cha 15:
Suala la kujifanya mtu mwingine kwenye mtandao, linaweza kuleta utata kwani kuna baadhi ya mitandao ambapo watumiaji hutumia majina ambayo sio ya kwao. Itakuwaje watu kwa madhumuni mabaya wakitafuta mtu mwenye jina kama hilo na kumshtaki mtumiaji wa mtandao?

Je, mtu kujifanya mtu mwingine inahusisha mtu kutumia jina lisilo lake hata kama hajajifanya mtu mwingine? Ni vema suala hili likafafanuliwa kisheria kwakuwa ni suala muhimu lakini wachache wataelewa manaa yake.

Kifungu cha 16:
Ni nani ana mamlaka ya kubainisha kuwa jambo lililowekwa kwenye mtandao ni la UKWELI, UONGO au UPOTOSHAJI? Ni wazi kuwa mamlaka husika inaweza tumia hili kama mtego kwa manufaa yao.

Kipengele hiki kama vingine kimeambatanisha muda usiopungua bila kusema muda usiozidi. Hivyo mtuhumiwa anaweza kufungwa hata kifungo cha maisha kutokana na mamlaka ya mahakama.

Watu binafsi wanaweza kutumia vibaya kifungu hiki kuzuia uhuru wa maoni kwa kuwaburuza watumiaji wa mtandao mahakamani kila kukicha na kuwapotezea muda wahusika ambao wanaweza kubainika mwishoni kuwa walionewa.

Kifungu cha 20:
Katika mawasililano ya mtandao kama ilivyo mawasiliano mengine kuna ujumbe ambao mtu hawezi kuacha kuupata

Mfano kutembea barabarani na kuona bango la matangazo, au kuwa ndani ya daladala iliyowasha redio.

Vivyo hivyo katika mtandao sio kila ujumbe anaopokea mpokeaji ameuomba na hivyo kifungu hiki kinafanya kila mtu atakayepokea ujumbe bila ridhaa yake kuwa amefanya kosa la jinai.

Kifungu cha 21(1):
Tafsiri za Kiswahili na kiingereza zipo tofauti kabisa.


Unknown Web Developer

No comments:

Post a Comment